Share
PUBLISHED ON August 28th, 2019

Changamoto soko la mazao ya wakulima lapatiwa muarobaini

Nasema bado una nguvu kwa sababu mbalimbali lakini kubwa ni mchango wake kwenye ustawi wa taifa na wananchi wake kwa ujumla.

Takwimu za karibuni zinaonyesha kwamba sekta ya kilimo inachangia asilimia 29.1 ya Pato la Taifa (GDP), asilimia 65.5 ya ajira kwa Watanzania wenye uwezo wa kufanya kazi, kati ya Watanzania takribani milioni 55 kwa hivi sasa.

Aidha, katika zama hizi za kuelekea Tanzania ya viwanda, kilimo kinatoa asilimia 65 ya malighafi za sekta ya viwanda na asilimia 30 ya mapato yatokanayo na mauzo ya nje ya nchi.

Na ndiyo maana serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli imechukua hatua mbalimbali kunyanyua kilimo ili kiwe na tija zaidi kwa wakulima wenyewe, wengi wakiwa wadogowadogo.

Imefanya hivyo kwa njia tofauti ikiwa ni pamoja na kufuta kodi na tozo zaidi ya 100 kwenye sekta hiyo, lakini pia kuwekeza zaidi katika mazao ya kipaumbele, yaani Pamba, Korosho, Tumbaku, Kahawa na Chai.

Aidha, inasisitiza juu ya umuhimu wa kuwa na kilimo cha kibiashara ili kutoa fursa ya wakulima, wengi wakiwa wadogo wadogo, kuongeza tija na hivyo kunyanyua hali zao za maisha.

Ndiyo ajenda ambayo imekuwa ikisimamiwa katika majukwaa takribani yote anayoyapata Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga, kama ilivyokuwa Julai 4 mwaka huu alipokuwa akizindua Bima ya Mazao kwa wakulima mkoani Simiyu.

Bima muhimu katika kukabiliana na hasara zitokanazo na vihatarishi vinavyoathiri uzalishaji.

Kimsingi jitihada hizi za serikali ya awamu ya tano zimeendelea kuleta tija kutokana na ongezeko la uzalishaji kwenye mazao mbalimbali ya kibiashara na yale yaliyo maalumu kwa ajili ya uhakika wa usalama wa chakula na lishe.

Ongezeko la uzalishaji kwenye zao la pamba ni mfano hai wa namna jitihada za serikali zinavyoonekana kuzaa matunda.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba (TCB), Marko Mtunga wakati wa uzinduzi rasmi wa msimu wa ununuzi wa pamba, Mei 2 mwaka huu, uzalishaji wa zao hilo unatarajiwa kuongezeka msimu huu hadi kufikia tani 400, 000 kutoka zaidi ya tani 200,000 za msimu uliopita.

Hiyo inaonyesha kwamba hatua zinazochukuliwa na Serikali kuboresha sekta ya kilimo zinazidi kuzaa matunda na hivyo kuwakwamua wakulima, wafugaji na wavuvi.

Hata hivyo katika ya jitihada hizi, bado kuna changamoto zinazohitaji kutatuliwa ili ajenda ya kuinua sekta ya kilimo iweze kuzaa zaidi matunda tarajiwa kwa maana ya kutoka katika kilimo cha kujikimu hadi cha kibiashara.

Zipo changamoto nyingi kama vile suala la kutegemea mvua, mabadiliko ya hali ya hewa, moto, magonjwa ya mimea kwa kutaja baadhi.

Hata hivyo katikati ya changamoto hizo, tafiti zilizofanywa na vyanzo mbalimbali ikiwamo Taasisi ya Utafiti, Sera na Uchumi (REPOA) zinaonyesha kwamba masoko ni changamoto kubwa zaidi baada ya mkulima kuwa amezalisha mazao yake.

Changamoto ya masoko ya mazao mbalimbali ya wakulima na hasa ya nje ya nchi ambako sehemu kubwa ya mazao yanayozalishwa yanauzwa inachangiwa na mengi, lakini kubwa yakiwa masuala ya muda na gharama.

Muda na gharama unaotumika kuomba vibali, leseni pamoja na vyeti vya usafi chini ya dirisha moja (single window system) kwa ajili ya kuuza mazao nje ama kuingiza bidhaa kama viuatilifu, mbolea na mbegu.

Kwa kuona changamoto hizo na hasa wakati ambapo Tanzania inalenga kuwa nchi ya viwanda ifikapo 2021 na ya kipato cha kati mwaka 2025, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Trade Mark East Africa, wamezindua mfumo ulio na suluhu dhidi ya changamoto hizo.

Kwa mujibu wa Ofisa Mfawidhi, Huduma ya Karantini na Usafi wa Mimea wa Wizara ya Kilimo, Daniel Katemani, Mfumo huu unaoitwa ATMIS (Agricultural Trade Management Information System), umeasisiwa na Watanzania.

Katemani anabainisha kwamba umekuwa na mafanikio makubwa toka ulipoanza kufanya kazi Mei mwaka huu, ingawaje ulizinduliwa rasmi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika Maadhimisho ya Sherehe za Nanenane, yaliyofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Nyakabindi, mkoani Simiyu.

“Umepunguza muda na gharama kwa wateja wetu na hivyo kuboresha na kurahisisha biashara ya kilimo na ndiyo maana sasa huwezi ukakuta msururu wa wateja pale bandarini, kama ilivyokuwa siku za nyuma,” anasema.

Anabainisha kuwa mfumo huu unahusisha taasisi za udhibiti na idara za serikali tano zilizo chini ya wizara ya kilimo ambazo ni pamoja na Sehemu ya Afya ya Mimea (PHS) kama inavyotambulika kwa wafanyabiashara wengi.

“Vilevile Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA), Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu (TOSKI), Kituo cha Utafiti na Uratibu wa Viuatilifu (TPRI) Arusha pamoja na Idara ya Usalama wa Chakula chini ya wizara ya kilimo,” anasema.

BODI

Kwa upande wa bodi zinazohusika katika mfumo huu, ofisa huyo mfawidhi anazitaja kuwa ni Bodi ya Pamba, Bodi ya Sukari, Bodi ya Chai na Bodi ya Mkonge Tanzania.

“Lakini pia Bodi ya Tumbaku, Bodi ya Korosho, Bodi ya Pareto na Bodi ya Kahawa,” anasema.

Katemani anafafanua kuwa taasisi, idara na bodi hizo za mazao ambazo ni mamlaka za uratibu zinawezeshwa kupitia mfumo wa ATMIS kupokea maombi na kutoa vibali kwa wafanyabiashara wanapotaka kupeleka mazao nje ama kuingiza bidhaa za kilimo nchini.

“Zamani ukitaka kupata leseni, vibali ama cheti cha usafi ni lazima uende kwenye ofisi za bodi ama taasisi husika, upewe fomu ili ukajaze, upewe namba ya udhibiti (control number) ili ukalipe benki,” anasema na kuongeza:

“Kisha urudi kwenye taasisi au bodi husika na fomu yako, uikabidhi hiyo fomu,  uambiwe njoo kesho ama kesho kutwa kwa sababu tunaifanyia kazi, kisha ikiwa tayari ndipo ukaichukue.”

Anabainisha, michakato yote hiyo ilimgharimu mteja muda na rasilimali za kwenda na kurudi.

“Sasa kama mteja yuko mbali na ofisi husika ilipo ilibidi asafiri… kwa mfano anahitaji kibali cha viuatilifu na yuko Mtwara, ilibidi aende Arusha ambako ndipo zipo ofisi za TPRI,” anasema.

Anabainisha kwamba kupitia mfumo huu wa ATMIS, mteja hahitaji kuingia gharama zote hizo bali ni suala la yeye kuingia katika mfumo huo unaopatikana kupitia kompyuta ama simu za mkononi.

“Unatuma maombi yako kwa njia ya mtandao, unajibiwa, unapewa namba ya udhibiti (control namba), unalipa kwa kutumia simu moja kwa moja kwenye mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato ya Serikali (GePG),” anasema na kuongeza.

“Njia hii inapunguza muda na gharama,” anasema.

FAIDA KWA SERIKALI

Kwa upande wa Serikali, Katemani anasema mfumo huu mpya unaongeza mapato ya serikali kwa sababu ya kuondoa kabisa tatizo la vibali feki lililokuwepo hapo nyuma.

“Matumizi ya vibali vya kizamani kwa maana vya kujazwa kwa mkono viliruhusu watu kuvighushi… kuna matukio ya bidhaa toka nchini kukamatwa nje ya nchi hapo zamani lakini vibali vilivyoruhusu usafirishaji wa bidhaa hizo havikuwa halali, vilighushiwa,” anasema na kuongeza:

“ATMIS imewekewa udhibiti kiasi kwamba mtu yeyote wa taasisi yoyote ya serikali kama TRA anaweza akaingia ndani ya mfumo na kujiridhisha kama kibali kimetolewa na serikali kwa maana ya taasisi ama bodi husika.”

MKURUGENZI TRADE MARK

John Ulanga, ni Mkurugenzi wa Trade Mark East Africa Tanzania ambayo imeshirikiana na wizara ya kilimo kuasisi mfumo huu.

Anasema wao kama shirika lisilolenga faida wanashirikiana na wadau, taasisi za serikali kuboresha mazingira ya kibiashara kwa kuhakikisha biashara nchini ikiwamo ya kilimo zinaboreshwa na kufanyika kwa njia rahisi na yenye ufanisi.

“Na ndiyo maana tumetumia takribani Sh. bilioni 1.6 kuhakikisha mfumo huu umeingia sokoni kwa kushirikiana na serikali…tunapata ufadhili kutoka nchi za  Uingereza, Norway na Ireland,” anasema.

Akizungumzia faida za ATMIS, Ulanga anasema pamoja na faida zingine mfumo unarahisisha upatikanaji wa taarifa za kibiashara zilivyofanyika kwa sababu inakuwa rahisi kuzipata tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.

“Kwa mfano serikali inapotaka taarifa kwamba katika kipindi cha mwezi mmoja ni vibali vingapi vimetolewa kwa ajili ya kusafirisha nini, kwa kiasi gani, vyenye thamani ya kiasi gani,” anasema na kuongeza:

“Taarifa hizo unaweza ukazipata ndani ya sekunde tu tofauti na ilivyokuwa huko nyuma ambapo ilikuwa inahitaji siku kadhaa kukaa na kufuatilia vibali vya mkono… hivyo inaongeza kasi ya upatikanaji wa taarifa kwa haraka ambazo zinaweza kutumiwa kufanya maamuzi.”

Ulanga anasema mfumo huu unaongeza ufanisi katika biashara ya kilimo, hivyo uwekezaji zaidi katika biashara ya kilimo kwa kuwa sasa kinachozalishwa kinalifikia soko kwa urahisi.

KUAMINIKA

Faida nyingine anayoitaja Ulanga ambayo imeanza kupatikana kupitia mfumo huu ni kuaminika kwa vyeti vinavyotoka Tanzania nje ya nchi.

“Hii ni kwa sababu vyeti kutoka kwenye mfumo wa ATMIS unaaminika zaidi tofauti na vyeti vilivyokuwa vikitolewa kwa njia ya mkono, ambavyo vilikuwa rahisi kughushiwa,” anasema.

MAFUNZO

Kwa upande wa mafunzo kwa wadau juu ya mfumo huu, Ulanga anasema walitoa mafunzo kwa wafanyabiashara takribani 300, wakiwamo mawakala wanaofanya biashara ya kupeleka au kuingiza nje mazao na bidhaa.

TPRI

Kwa upande wake Nelson Kawishe ambaye ni Ofisa Tehama wa Kituo cha Utafiti na uratibu wa viuatilifu (TPRI) kilichoko Arusha anasema mfumo huo umekisaidia kituo kuwa na data za kielektroniki kwa ajili ya wadau kwa maana ya wauzaji na wasafirishaji.

“Kwamba ukitaka kupata taarifa za hawa wadau, unabofya tu unapata kila kitu ikiwamo mahali mteja alipo,” anasema.

Aidha anabainisha faida nyingine iko kwa upande wa serikali, taasisi na kwa wakulima.

“Siku za nyuma kulikuwa na uingizaji wa bidhaa feki kwani mfanyabiashara aliweza kuingiza viautilifu vilivyo chini ya viwango, lakini sasa hilo halipo kwa sababu ni rahisi kufuatilia kilichoagizwa kama kinaendana na matakwa ya mkulima,” anasema na kuongeza:

“Ina maana mfanyabiashara ataruhusiwa kuingiza viuatilifu vilivyo vya viwango, kwani visivyo na viwango vinarudishwa palepale bandarini.”

Kawishe anasema hiyo inawezekana kwa sababu kupitia katika mfumo wanamtaka muigizaji apeleke sampuli ya viatilifu, viingizwe kwenye maabara kama vinakidhi viwango.

“Kama vinakidhi anapewa cheti cha uchambuzi wa sampuli cha kukidhi viwango, ndipo anapata cheti kinachomruhusu kuingiza.. hivyo sasa hivi hakuna njia za panya kama ilivyokuwa huko nyuma,” anasema.

Anabainisha kwamba kupitia ATMIS hakuna mkulima atakayepata viautilifu vilivyo chini ya viwango.

WATEJA

Mtaalamu huyo anabainisha wateja wakubwa wa TPRI kuwa ni pamoja na bodi zote za mazao na hata serikali kwa sababu kuna wakati hununua viautilifu kwa ajili ya wakulima kama ruzuku.

“Lakini maduka yote yanayouza viualitifu rejareja  na yale ya jumla ni wateja wetu, pia waagizaji wote wa viualitifu nchini  na  kampuni zote za fumigation, viwanda vinavyotengeneza sumu ni wateja wetu.

WAFANYABIASHARA

Joseph Baltazari ni mfanyabiashara anayesafirisha nje marobota ya pamba.

Anasema kabla ya mfumo huu kuanzishwa changamoto zilizokuwapo zamani zilikuwa ni pamoja na muda wa kupata vibali lakini pia uwapo wa vibali vingi vya kughushi.

“Kupata kibali zamani ilikuwa inaweza ikakuchukua mpaka siku 20…ujaze fomu, upate namba ya udhibiti (control number), uwasilishe nyaraka, uende benki kulipia na taratibu chungu nzima,” anasema na kuongeza:

“Sasa usahihi umeongezeka, hakuna suala la kwenda na kurudi, hivyo inaokoa muda na gharama kwa sababu vyote hivyo unaomba kwenye mtandao kupitia mfumo wa ATMIS, unafanyiwa uchambuzi mtandaoni, kisha unafanya malipo yako mtandaoni hata kwa njia ya simu…ni muda mfupi sana.”

Anasema mfumo huu umewaondolea muda mrefu wa kusubiri lakini pia gharama za kushughulikia mchakato mzima wa kupata vibali.

“Ninaona kuna nuru kubwa katika biashara ya kilimo nchini na hivyo tija kwa ustawi wa taifa,” anasema.

Source: IPPMEDIA

Disclaimer: The views and opinions expressed in this article are those of the authors and do not necessarily reflect the official policy or position of TradeMark Africa.